TSB YAFANIKIWA KUUZA MKONGE KWENYE NCHI TAKRIBANI 26 DUNIANI
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) Bw.Saddy Kambona amesema hali ya masoko Katika zao la mkonge ni nzuri kwa sababu bei ziko vizuri, na kuanzia mwaka 2021 mpaka hivi sasa wamefanikiwa kuuza mkonge kwenye nchi takribani 26 na mnunuzi mkuu wa mkonge ni China.
.
Kambona amesema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo na mwelekeo kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 leo Agosti 16, 2023 katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma.
.
Amesema kwa kipindi cha Mwaka Jana 2022 waliweza kukusanya na kusambaza Miche 6,991,200 ya mbegu za Mkonge bure kwa wakulima wadogo katika Wilaya 16 za Korogwe,Muheza, Tanga, Mkinga, Handeni, Kilindi, Rorya, Bunda, Butiama, bariadi, Bagamoyo(Chalinze), Kisarawe, Mkuranga, Manyoni(Itigi), Singida Vijijini na Mkalama.
.
"Takwimu zinaonesha hadi mwaka 2020, bodi iliweza kusajili wakulima wadogo 6887, Mwaka 2022 idadi ya wakulima wadogo waliosajiliwa ni 8972 na hata hivyo wakulima wadogo wa Mkonge ambao hawajafikiwa na kusajiliwa na TSB wanakadiriwa kufikia 22,000" amesema Kambona.
.
Mkurugenzi mkuu huyo amesema wanatarajia kuanzisha vituo vya uchakataji wa zao hilo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wadogo ambao wamehamasika kufanya kilimo hicho na mkonge wao utaanza kuvunwa mwakani 2024.
.
Kambona amesema Kuanzia mwaka 2020 walizalisha tani 37,022 za Singa za Mkonge walizalisha, 2021 uzalishaji uliongezeka hadi kufikia tani 39,484, 2022 walifikia tani 48,351 na mwaka huu 2023 wamefikia tani 34,630.
.
"Tumeweka lengo mwaka huu kufikisha tani 60,000 angalau tuwe katikati ya lengo kuu la kufikisha 120,000 Ifikapo Mwaka 2025-26".
.
Aidha,Kambona amesema kwa hivi sasa Tanzania ni nchi ya pili duniani katika uzalishaji wa zao la mkonge, huku nchi ya Brazil ikishika nafasi ya kwanza na hii ni kutokana na uhamasishaji mkubwa walioufanya kwa wakulima hapa nchini.
.
"Brazil hawana mashamba Makubwa kama huku kwetu, sehemu kubwa ya Kilimo cha Mkonge kinalimwa na wakulima wadogo" amesema.
#JordanMediaupdates
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

