logo

TAEC YAANZA KWA USHINDI WA MICHEZO MIWILI SHIMMUTA MOROGORO

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeanza kwa kishindo mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) yanayofanyika mkoani Morogoro, baada ya kuibuka na ushindi katika michezo yake miwili ya awali ya mpira wa miguu.

‎

‎Katika michezo hiyo, timu ya TAEC imeonesha kiwango kizuri kwa kuifunga Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) kwa mabao 2-1, kabla ya kuendeleza ubabe wake kwa kuichapa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa mabao 2-1.

‎

‎Ushindi huo umeipa TAEC mwanzo mzuri na kuongeza ari na morali kwa wachezaji wake, huku timu hiyo ikiendelea kujipanga kuhakikisha inafanya vizuri katika michezo inayofuata, ikiwa na dhamira ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo mwaka huu.

‎

‎Akizungumzia ushiriki wa TAEC katika mashindano hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Tume, Dkt. Jerome Mwimanzi, amesema ushiriki huo ni sehemu ya jitihada za uongozi wa TAEC, chini ya Mkurugenzi Mkuu, Prof. Najat Kassim Mohammed, za kuimarisha afya za wafanyakazi, kukuza mshikamano na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

‎

‎Dkt. Mwimanzi ameongeza kuwa, pamoja na kuimarisha afya na mahusiano miongoni mwa wafanyakazi, mashindano hayo yanatoa fursa muhimu ya kuitangaza TAEC na kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine kupitia sekta ya michezo.

‎

‎Mashindano ya SHIMMUTA mwaka huu yanashirikisha zaidi ya taasisi na mashirika 100 kutoka maeneo mbalimbali nchini, zikichuana katika michezo tofauti. Mashindano hayo yameanza Novemba 6, 2026, mkoani Morogoro na yanatarajiwa kuhitimishwa Novemba 21, 2026.

‎

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn