BoT YAIMARISHA MIFUMO SALAMA YA MALIPO NCHINI
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema imeendelea kuimarisha mifumo ya malipo ya taifa kwa lengo la kuongeza usalama, kupunguza gharama za miamala, kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan waliopo maeneo ya vijijini.
Hayo yamesemwa jana na Mchambuzi Mwandamizi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Doto Namkaa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Namkaa alisema BoT ndiyo msimamizi mkuu wa mifumo ya malipo nchini na imeweka mifumo mbalimbali inayowezesha miamala kufanyika kwa usalama na ufanisi, ikiwemo mfumo wa malipo makubwa (Tanzania Interbank Settlement System - TISS), pamoja na mifumo ya malipo madogo inayounganisha benki, taasisi za fedha na watoa huduma za fedha kwa njia ya simu.
Alifafanua kuwa mifumo hiyo inatumika kuwezesha miamala ya taasisi za fedha, malipo ya mishahara ya watumishi wa umma, pamoja na uhamishaji wa fedha kati ya benki na mitandao ya simu kwa haraka na usalama.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana, Namkaa alisema Ripoti ya BoT ya mwaka 2025 inaonesha ongezeko kubwa la mawakala wa huduma za kifedha, ambapo idadi yao imeongezeka kwa asilimia 34 na kufikia takribani mawakala 94,000, hatua ambayo imeongeza upatikanaji wa huduma za kifedha hasa katika maeneo ya vijijini.
Aidha, alisema idadi ya wafanyabiashara wanaokubali malipo ya kidijitali imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 80 kutokana na matumizi ya mfumo wa Tanzania QR, unaowawezesha wafanyabiashara kupokea malipo kwa njia ya simu kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
"Kwa sasa Tanzania ina zaidi ya watumiaji wengi wa huduma za simu za mkononi, hali inayoonesha kuwa wananchi wengi wamefikiwa na huduma za fedha kidijitali na hivyo kuongeza ujumuishaji wa kifedha nchini," alisema.
Hata hivyo, Namkaa alikiri kuwa pamoja na mafanikio hayo bado zipo changamoto zinazohitaji kushughulikiwa, ikiwemo unyeti wa wananchi kuhusu gharama za miamala na ongezeko la matukio ya udanganyifu wa kifedha kupitia mifumo ya kidijitali.
Alisema BoT imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kupunguza gharama za huduma za malipo kwa kuweka viwango vinavyolinda watumiaji, ikiwa ni pamoja na kupunguza ada kwa miamala midogo na kuweka ukomo wa tozo kwa baadhi ya miamala ili huduma ziwe nafuu zaidi kwa wananchi.
Katika kukabiliana na udanganyifu wa kifedha, Namkaa alisema BoT imeimarisha mifumo yake kwa kutumia viwango vya kimataifa vya usalama vya ISO 20022, vinavyowezesha kubaini miamala yenye viashiria vya hatari mapema na kuzuia uhalifu wa kifedha.
Alisema pamoja na matumizi ya teknolojia, BoT hufanya ukaguzi wa moja kwa moja kwa watoa huduma za malipo, hufuatilia taarifa za miamala kila siku na kuhakikisha taasisi zote zinazotoa huduma za fedha zinazingatia sheria na kanuni za usalama wa mifumo ya malipo.
"Elimu kwa umma ni sehemu muhimu ya mapambano dhidi ya udanganyifu.
" Tunawaelekeza wananchi kutotoa namba zao za siri (PIN) , kuhakikisha wanathibitisha taarifa za mpokeaji kabla ya kutuma fedha, na kuripoti mara moja kwa mtoa huduma au Benki Kuu endapo watakumbana na vitendo vya udanganyifu," alisema.
Aidha, alisema BoT imekuwa ikitumia maonesho ya biashara, mitandao ya kijamii na programu mbalimbali za elimu kwa umma kuendelea kutoa uelewa kuhusu matumizi salama ya huduma za kifedha kidijitali.
Namkaa pia alisema mafanikio ya Tanzania katika sekta ya mifumo ya malipo yameendelea kutambulika kimataifa, ambapo mwaka 2025 nchi ilipokea tuzo ya Financial Inclusion Innovation Award kutokana na ubunifu katika kukuza ujumuishaji wa kifedha, kupunguza gharama za miamala na kuwezesha matumizi ya mfumo wa TANQR.
Aliongeza kuwa mafanikio hayo yameifanya Tanzania kuwa mfano kwa nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Kenya, Rwanda, Uganda na Lesotho, ambazo zimekuwa zikifika nchini kujifunza namna mifumo ya malipo ya Tanzania ilivyoboreshwa na kusimamiwa.
Alisisitiza kuwa BoT itaendelea kushirikiana na wadau wote wa sekta ya fedha kuhakikisha mifumo ya malipo nchini inakuwa salama, jumuishi, nafuu na inayokidhi viwango vya kimataifa kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa Taifa.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

