BMH, JKCI WAZIBA MATUNDU YA MOYO KWA WATOTO WA BURUNDI
Madaktari bingwa bobezi kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na madaktari Bingwa bobezi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mara ya kwanza wamekamilisha kambi ya upasuaji wa kuziba matundu ya moyo kwa watoto kutoka nchini Burundi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa BMH, Prof. Abel Makubi katika mkutano na waandishi wa habari ambapo umesema ushirikiano kati ya BMH na JKCI utaendelea kuimarishwa ili kupanua wigo wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi wa kutoa huduma bora kwa wananchi, pamoja na kusaidia kukuza tiba utalii nchini.
“Hatua hii imekuwa ya kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa BMH kwa kushirikiana na JKCI kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka nje ya Tanzania, jambo hili ni hatua muhimu katika kukuza tiba utalii na huduma za kibobezi nchini”, amesema Prof. Makubi.
Prof. Makubi ameongeza kuwa haikuwa jambo jema kuona wananchi wa Tanzania na nchi za jirani wakisafiri kwenda nje ya mbali sana kutafuta matibabu wakati Tanzania ina wataalamu wenye uwezo wa kutoa huduma hizo. Tunataka kuona wagonjwa kutoka nchi mbalimbali wanapata huduma hizi hapa nchini na kwa gharama nafuu, badala ya kwenda nje za mbali kutafuta matibabu haya.
Akizungumza baada ya matibabu hayo, Dk. Ahmed Toure, bingwa wa upasuaji wa moyo na kifua amesema wagonjwa hao walikuwa na changamoto za kuzaliwa na matatizo ya muundo wa moyo ambayo yalihitaji matibabu maalumu ili moyo uweze kufanya kazi kwa ufanisi na baadhi ya watoto huzaliwa wakiwa na matatizo ya mishipa ya moyo ambapo damu haiendi kwenye mapafu na mwilini kwa uwiano unaotakiwa.
“Tatizo hili linaweza kusababisha madhara makubwa kwa mapafu endapo mtoto hatapatiwa matibabu kwa wakati. Baadhi ya watoto wakifikisha umri wa miezi sita hadi mwaka mmoja wanaweza kuanza kupata madhara makubwa, na kufanya upasuaji baadaye huwa changamoto zaidi na kwa watoto wanaopata matibabu sahihi na mapema, uwezekano wa kuendelea kuishi maisha marefu huongezeka na baadhi wanaweza kuishi hadi miaka 30 au zaidi kulingana na hali zao.,” amesema Dkt. Toure.
Dk. Asha Mahita, Mratibu wa Tiba Utalii Tanzania, alisema serikali kupitia Dira ya Maendeleo 2050 imelenga kuhakikisha huduma za tiba utalii zinakuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya afya.
Alisema hatua ya kuwahudumia wagonjwa kutoka Burundi ni ushahidi kuwa Tanzania inaendelea kujenga uwezo wa kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa kiwango cha kimataifa.
“Haikuwa rahisi kuwaleta wagonjwa kutoka nchi nyingine na kuwapatia matibabu salama. Jambo muhimu sasa ni kuhakikisha wanaendelea kufuatiliwa baada ya matibabu,” alisema Dkt. Mahita
Naye Dk. Godwin Godfrey kutoka JKCI, ambaye ni bingwa mbobezi wa upasuaji wa moyo kwa watoto, amesema wamefurahishwa na namna BMH inavyoendelea kupanua huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.
“Ni muhimu taasisi kubwa kama hizi kuendelea kushirikiana kwa sababu kufanya hivyo kunasaidia wataalamu kupata nafasi ya kujifunza na kuongeza uwezo wao, huku wakisaidia wagonjwa wengi zaidi kupata huduma karibu na maeneo yao hata wananchi wasiojiweza kupata huduma bora,” amesema Dkt.Godfrey.
Kwa upande wa Burundi, Dk. Nzitunga Aimee Jean Carmen Octavie kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Gitega, alisema wamefurahi kuona Tanzania ikiweza kutoa huduma hizo kwa kuwa nchi hizo mbili zina uhusiano wa karibu.
Alitoa shukrani kwa madaktari na uongozi wa BMH kwa kuwapatia wagonjwa wao matibabu salama.
Mzazi wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji, Shedrack Nzigiyimana, alisema ana furaha kubwa kutokana na maendeleo ya afya ya mtoto wake baada ya kupata matibabu.
Ameshukuru Serikali ya Tanzania na BMH kwa moyo wa upendo waliouonyesha, akisema ujirani mwema kati ya Tanzania na Burundi umewezesha watoto wao kupata huduma muhimu.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

