logo

HALMASHAURI ZATAKIWA KUSIMAMIA KIKAMILIFU MASUALA YA TAKA NGUMU PAMOJA NA UTEKELEZAJI WA MASHARTI YA VIBALI VYA BURUDANI MNAVYOTOA KUDHIBITI KELELE CHAFUZI

‎Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limezitaka Halmashauri nchini kusimamia kikamilifu ukusanyaji na utupaji wa taka ngumu pamoja na kuhakikisha masharti ya vibali vya burudani wanavyotoa yanazingatiwa ili kudhibiti kelele chafuzi na kulinda afya za wananchi. Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa NEMC, Bi. Martha Kawishe, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

‎Amesema usimamizi wa kelele na mitetemo unasimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191 pamoja na Kanuni za Udhibiti wa Kelele na Mitetemo za mwaka 2015. NEMC ina jukumu la kufanya ukaguzi, kupima viwango vya kelele, kutoa maelekezo ya maboresho na kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu changamoto za mazingira.

‎Bi. Kawishe amefafanua kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zina wajibu wa kusimamia leseni na vibali vya burudani pamoja na kuhakikisha masharti yaliyoainishwa yanafuatwa. Aidha, OSHA inafuatilia athari za kelele kwa afya za wafanyakazi huku Jeshi la Polisi likisaidia utekelezaji wa sheria na kudumisha utulivu wa jamii pale kunapojitokeza ukiukwaji wa sheria.

‎NEMC imewataka waendeshaji wa biashara, viwanda, maeneo ya burudani, nyumba za ibada na shughuli za ujenzi kuzingatia viwango vya kelele vilivyowekwa kisheria na kutumia mbinu za kupunguza uchafuzi wa mazingira. Vilevile, wananchi wamehimizwa kuwasilisha malalamiko ya taka, kelele na changamoto nyingine za mazingira kwa mamlaka husika ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn