logo

SHERIA NDOGO 229 ZATAFSIRIWA KISWAHILI KUIMARISHA UELEWA WA SHERIA

Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imeendelea kuimarisha upatikanaji wa haki na uelewa wa sheria kwa wananchi kwa kukamilisha tafsiri ya sheria kuu 433 kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili.

‎.

‎Hatua hiyo imefikisha jumla ya sheria kuu 446 zinazopatikana kwa lugha ya Kiswahili hadi kufikia Machi 2026.

‎.

‎Sheria hizo zilitangazwa rasmi kupitia Tangazo la Serikali Na. 659 la mwaka 2025 na sasa zinatumika kuwezesha utoaji wa haki kwa lugha ya Kiswahili na kuwasaidia wananchi kuelewa sheria za nchi kwa urahisi.

‎.

‎Akizungumza Aprili 24, 2026, Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, alisema kuwa wizara kupitia OCPD inaendelea na tafsiri ya sheria ndogo ili kukamilisha utekelezaji wa sheria hizo kwa Kiswahili.

‎.

‎Alieleza kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya sheria ndogo 229 zimetafsiriwa kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili.

‎.

‎Aidha, ofisi hiyo imeendelea na majukumu ya kuandaa miswada ya sheria, kusimamia uchapishaji wa sheria ndogo, pamoja na kutafsiri na kurekebisha sheria mbalimbali.

‎.

‎Katika kipindi hicho, OCPD imeandaa miswada minne ya sheria, ambapo miwili tayari imesomwa kwa mara ya kwanza Bungeni.

‎.

‎Miswada hiyo ni Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2026 na Muswada wa Sheria ya Mikopo kwa Dhamana za Mali Zinazohamishika wa Mwaka 2026.

‎.

‎Vilevile, ofisi hiyo imeandaa, kuhakiki na kuchapisha jumla ya sheria ndogo 447, zikiwemo kanuni 107, notisi 145, amri 125, sheria ndogo 62, hati saba na muongozo mmoja.

‎.

‎Sambamba na hilo, OCPD imekamilisha Toleo la Urekebu la Nyongeza la Mwaka 2025, lililojumuisha sheria kuu 71 zilizorekebishwa pamoja na sheria ndogo 265 zilizofanyiwa urekebu, hatua inayolenga kuimarisha ubora, usahihi na upatikanaji wa sheria nchini.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn