KLINIKI TEMBEZI KUHUDUMIA WANAWAKE MILIONI 14 KANDA YA KATI
Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb.) amezindua gari maalumu lenye kliniki tembezi ya Magonjwa ya Saratani kwa Wanawake katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH).
Mhe. Mchengerwa ametumia nafasi hiyo kuwataka Watumishi wa Afya nchini kuendelea kufanya kazi kwa bidii, moyo wa kujitoa na maaarifa katika kuwahudumia watanzania wanaowategemea na kusisitiza kuwa huduma za Afya zinahitaji kujitolea sana katika kuhudumia wananchi.
"Jiepusheni na vitendo viovu vinavyoweza kuichafua BMH na Serikali kwa ujumla kama vitendo vya Rushwa. Tuwe na huduma bora kwa mteja, lugha nzuri; Mkurugenzi Mtendaji endelea kuwakumbusha watumishi kila wakati juu ya Wajibu wao, vikao vya kukumbusha majukumu na wajibu wa watumishi wote viendelee kufanyika" alisisitiza Mhe. Mchengerwa
Alitaka watamushi wa BMH kutambua kuwa wana wajibu wa kufanya kazi asubuhi, mchana na usiku ili matokeo yaonekane ambayo yatasaidia na kuwashawishi watoa maamuzi katika mchakato wa kuipandisha hadhi BMH kuwa Hospitali ya Taifa.
Kwa upande wake Mratibu Mkazi wa mradi mtambuka wa Saratani za wanawake Afrika Mashariki Dkt. Sara Maongezi amesema kuwa mradi huo ni wa miaka minne (4) kuanzia mwaka 2025 huku ukiangazia kupunguza madhara yatokanayo na saratani kwa wanawake ikiwemo kuboresha vituo vya saratani na kugawa vifaa vya matibabu ya saratani ikiwemo kliniki hiyo tembezi yenye thamqni ya shilingi Mil 272.
"Tunagawa Kliniki tembezi kwa ajili ya kuwezesha uchunguzi wa saratani ya shingo ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti kwenye maeneo ya vijijini ambako wakina mama hawawezi kufika Hospitali kwa urahisi kwa kuwa gari hiyo ina vifaa vyote muhimu" alisisitiza Dkt. Sara Maongezi.
Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi amesema kuwa mradi huu ni muendelezo wa makubaliano ya ushirikiano (MOU) ambao tulisaini na Taasisi ya Afya ya Aga Khan mwaka jana kwenye maeneo ya mafunzo, utafiti na matibabu, mradi utasaidia kuhudumia wananchi takribani mil 14 wa mikoa ya Dodoma na inayozunguka Kanda ya Kati.
"Itasaidia kuweza kuwafanyia Wanawake uchunguzi na kutambua mapema kama wana magonjwa ya Kansa, kuwapa matibabu stahiki na kutoa elimu ya Kansa kwa jamii; mradi utasaidia mafunzo ya kuwajengeaa uwezo watoa huduma wawili wa BMH ili waweze kwenda kutoa huduma kwa jamii" alisisitiza Prof. Makubi.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

