USHIRIKIANO TANZANIA NA CHINA WAIMARISHA HUDUMA ZA AFYA BMH
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma, leo Aprili 17, 2026 imepokea timu ya madaktari bingwa wabobezi watano kutoka China watakaotoa huduma katika hospitali hiyo ya rufaa ya kanda kwa kipindi cha miaka miwili.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi, ameishukuru Serikali kwa kuwezesha ujio wa wataalamu hao, akisema wataongeza uwezo wa hospitali kupanua wigo na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
.
Ameeleza kuwa timu hiyo inajumuisha madaktari bingwa katika fani za Tiba Asili ya Kichina, Upasuaji wa Ubongo, Mishipa ya Fahamu na Uti wa Mgongo, Upasuaji wa Mikono na Miguu, Upasuaji wa Mifupa pamoja na magonjwa ya Moyo, na kwamba watapangiwa katika idara mbalimbali kulingana na utaalamu wao.
“Taasisi itawapatia ushirikiano mkubwa katika kipindi chote watakachokuwa wakihudumu hapa BMH,” alisema Prof. Makubi.
Kwa upande wake, Kiongozi wa msafara wa madaktari hao kutoka China, Liu Jia, amesema amefurahishwa kupata fursa ya kufanya kazi na BMH kwa mara ya kwanza, akibainisha kuwa programu hiyo ni matokeo ya uhusiano mzuri wa kidiplomasia wa muda mrefu kati ya Tanzania na China.
.
"Programu hii ni matokeo ya uhusiano mzuri wa kidiplomasia wa muda mrefu kati ya Tanzania na China," alisema Dkt. Jia.
.
Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Ndg. Marcelo Kaijage, amesema ushirikiano wa sekta ya afya kati ya Tanzania na China umekuwa na manufaa makubwa, na kuwataka Watanzania kujitokeza kupata huduma kutoka kwa wataalamu hao watakaoshirikiana na madaktari wa ndani.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

