logo

NDOINYO ATOA WITO NGORONGORO IGAWANYWE,NA MIUNDOMBINU IBORESHWE ILI KURAHISISHA HUDUMA

Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Yanick Ndoinyo, ameishauri Serikali kugawa Wilaya ya Ngorongoro na kuboresha miundombinu yake ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

‎Akizungumza bungeni,wakati akichangia hotuba ya Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma, Ndoinyo alisema Wilaya ya Ngorongoro yenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba 14,030 inawakabili wananchi na changamoto kubwa ya umbali, hali inayowalazimu kusafiri hadi kilomita 300 kufuata huduma katika makao makuu ya wilaya.

‎Amesema kutokana na jiografia na mgawanyo wa maeneo, ipo haja ya kuanzisha halmashauri mpya pamoja na maeneo mengine ya kiutawala ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

‎“Wananchi wanapohitaji huduma muhimu kama vitambulisho vya NIDA, vyeti vya kuzaliwa na nyaraka nyingine, hulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda wilayani. Hali hii inapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka,” amesema Ndoinyo.

‎Aidha, ameeleza kuwa Wilaya ya Ngorongoro ni miongoni mwa wilaya chache nchini ambazo hazijaunganishwa na barabara ya lami kuelekea Mkoa wa Arusha, hali inayochangia kutengwa kimaendeleo.

‎Mbunge huyo alisisitiza umuhimu wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mto wa Mbu hadi Loliondo, akibainisha kuwa kukamilika kwake kutapunguza muda wa safari kutoka saa 12 hadi kati ya saa mbili hadi tatu.

‎Kuhusu uchumi wa wilaya hiyo, Ndoinyo amesema unategemea sekta kuu tatu ambazo ni ufugaji, kilimo na utalii, huku akieleza kuwa sekta ya utalii bado haijatumika kikamilifu licha ya kuwa na mapato makubwa yanayofikia zaidi ya shilingi milioni 260.

‎Ameitaka Serikali kuongeza juhudi katika kuendeleza utalii ili uweze kunufaisha wananchi na taifa kwa ujumla, sambamba na kuimarisha sekta za uzalishaji hasa kilimo na ufugaji.

‎“Kwa Ngorongoro, ufugaji si tu uchumi bali pia ni sehemu ya mila na desturi. Ni muhimu kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wafugaji wanapata malisho ya kutosha wakati wote wa mwaka ili kuepuka vifo vya mifugo wakati wa kiangazi,” alisisitiza.

‎Ameongeza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mifugo na Uvuvi inapaswa kuweka mikakati ya kudumu ya upatikanaji wa malisho ili kulinda uchumi wa wafugaji.

‎Kwa upande wa kilimo, alisema takribani wananchi 13,000 wanajishughulisha na shughuli hiyo, na kuipongeza Serikali kwa kutoa mbegu na mbolea za ruzuku kwa wakati. Hata hivyo, alibainisha kuwa changamoto kubwa ni ukosefu wa masoko na miundombinu ya uhifadhi wa mazao.

‎“Sehemu kubwa ya mazao hupotea shambani au njiani wakati wa kuyapeleka sokoni. Ni muhimu Serikali ikawekeza katika miundombinu ya uhifadhi ili kulinda mazao na kipato cha wakulima,” alisema.

‎Pia aligusia changamoto ya mifugo kutaifishwa inapovamia maeneo yaliyohifadhiwa, akiiomba Serikali kusitisha utaratibu huo na badala yake kutafuta suluhisho rafiki kwa wafugaji.

‎“Naiomba Serikali kupitia sekta husika kuacha kutaifisha mifugo ya wananchi kwani mingi ina wenyewe, hatua hiyo inaathiri uchumi wao,” amesisitiza.

‎Katika hatua nyingine, Ndoinyo amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiongoza nchi kwa mafanikio, akieleza kuwa Tanzania imeendelea kuwa na utulivu, amani na kuvutia mataifa mengine barani Afrika.

‎Aidha, amezipongeza taasisi za umma kwa kuendelea kuimarika, akirejea ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinazoonesha uwazi na uhuru katika utendaji wa taasisi hizo.

‎Amempongeza Waziri Mkuu kwa hotuba yake iliyoeleza mafanikio ya Serikali pamoja na Dira na mipango ya maendeleo.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn