MSHAIRI ABDILATIF ABDALLA MGENI RASMI TUZO ZA UANDISHI BUNIFU APRIL 13,2026 JIJINI DAR ES SALAAM
Hafla ya Nne ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu inatarajiwa kufanyika Aprili 13, 2026 katika ukumbi wa Super Dome jijini Dar es Salaam.
.
Akizungumza jijini Dodoma Aprili 8, 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema tuzo hiyo hufanyika kila mwaka kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na kutambua mchango wake mkubwa katika kukuza lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Taifa.
.
"Mashindano ya mwaka huu yamejikita katika nyanja nne za fasihi ambazo ni riwaya, hadithi za watoto, tamthiliya na ushairi, zikilenga kuibua vipaji vipya na kuendeleza ubunifu wa waandishi wa Kitanzania" alisema Prof. Mkenda.
.
Amesisitiza kuwa tuzo hiyo inalenga kukuza matumizi ya Kiswahili, kuendeleza vipaji vya uandishi bunifu, kulinda historia na utamaduni wa Taifa, pamoja na kuongeza idadi ya vitabu vinavyohifadhiwa kwenye maktaba mbalimbali nchini.
.
Mgeni rasmi wa hafla hiyo anatarajiwa kuwa mshairi mashuhuri duniani, Abdilatif Abdalla, mwenye asili ya Afrika Mashariki ambaye aliwahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 15.
.
Hafla hiyo itatanguliwa na mjadala wa kitaaluma utakaowakutanisha waandishi bunifu kutoka Tanzania pamoja na wageni waalikwa kutoka Uganda na Rwanda kwa lengo la kubadilishana uzoefu na maarifa ya kifasihi.
.
Aidha, Prof. Mkenda ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza zaidi ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuchapisha na kusambaza vitabu vilivyoshinda tuzo hiyo, hatua inayolenga kuhamasisha utamaduni wa usomaji na kukuza sekta ya uchapishaji nchini.
.
Tangu kuanzishwa kwa tuzo hiyo, jumla ya Watanzania 27 wameshinda, huku washiriki wakijitokeza kutoka ndani na nje ya nchi, zikiwemo Kenya, Jamhuri ya Czech na Australia.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

