logo

BMH KUKUSANYA BILIONI 7 KUWATIBU WAGONJWA 100 WA SELI MUNDU NA FIGO

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma imezindua mpango maalum wa kukusanya Shilingi Bilioni 7 ndani ya miaka miwili kwa lengo la kugharamia matibabu ya watu 100 wanaohitaji upandikizaji wa viungo muhimu, wakiwemo watoto wenye ugonjwa wa seli mundu wanaohitaji kupandikizwa uloto na wagonjwa wa figo wanaohitaji kupandikizwa figo.

‎Akizungumza na waandishi wa habari Machi 31, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi, amesema fedha hizo zitapatikana kupitia harambee itakayofanyika Mei 08, 2026 jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya hospitali hiyo.

Mgeni rasmi katika harambee hiyo anatarajiwa kuwa Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

‎Kwa mujibu wa Prof. Makubi, watoto 50 wanatarajiwa kupandikizwa uloto ili kupona kabisa ugonjwa wa seli mundu, huku wagonjwa wengine 50 wakipandikizwa figo kama tiba kamili ya ugonjwa wa figo.

Ameeleza kuwa gharama ya upandikizaji wa uloto kwa mtoto mmoja ni takribani Sh75 milioni hapa nchini, ikilinganishwa na Sh120150 milioni endapo matibabu hayo yatafanyika nje ya nchi.

Kwa wagonjwa wa figo, upandikizaji hugharimu takribani Sh40 milioni kwa mgonjwa mmoja, tofauti na uchujaji wa damu wa mara tatu kwa wiki unaogharimu fedha nyingi kwa muda mrefu.

‎Amesema tatizo la seli mundu ni kubwa nchini ambapo takribani watoto 12,000 huzaliwa kila mwaka na ugonjwa huo, huku kukiwa na idadi ya wagonjwa wa figo wanaohitaji upandikizaji kama suluhisho la kudumu badala ya kuendelea na uchujaji wa damu.

Prof. Makubi ameongeza kuwa hadi sasa BMH imefanikiwa kufanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 55, ambapo wote wameendelea vizuri isipokuwa mmoja aliyepata changamoto zisizohusiana na upasuaji huo.

Pia watoto 28 kutoka ndani na nje ya nchi wamepandikizwa uloto na kupona seli mundu kwa gharama ya jumla ya Sh1.9 bilioni.

‎Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dk. David Mwenisano, amesema gharama za uchujaji wa damu kwa wagonjwa wa figo ni kubwa mno.

Amefafanua kuwa mtoto anayelipia bima ya afya ya Sh50,400 kwa mwaka akipata tatizo la figo anaweza kutumia hadi Sh28 milioni kwa mwaka kwa uchujaji wa damu — sawa na michango ya watoto 571 kwa mwaka.

‎Amesema hali hiyo ndiyo iliyosababisha serikali kuanzisha mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ambapo kaya maskini takribani milioni 3.9 zinatarajiwa kugharamiwa bima na serikali.

Katika awamu ya kwanza, kaya 276,004 tayari zimeshasajiliwa kwa gharama ya Sh41 bilioni kwa mwaka.

‎Uongozi wa BMH umetoa wito kwa taasisi za umma na binafsi, wadau wa maendeleo na watu binafsi kujitokeza kwa wingi kushiriki harambee hiyo ili kusaidia matibabu ya wagonjwa wasioweza kumudu gharama hizo.

‎#JordanMediaUpdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn