MAFUNZO YA UKUSANYAJI TAARIFA ZA RASILIMALI BARABARA YAFUNGULIWA ARUSHA
SERIKALI kupitia Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), imefungua rasmi mafunzo maalum kuhusu mwongozo wa ukusanyaji wa taarifa za rasilimali za barabara yanayofanyika mkoani Arusha.
.
Huku Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga, akiagiza mifumo yote ya usimamizi wa rasilimali za barabara, ijengwe kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, hususani ISO 55000, ili kuhakikisha ufanisi, uwazi na uendelevu katika usimamizi wa miundombinu hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
.
Mafunzo hayo yamewashirikisha wataalamu kutoka Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) pamoja na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS).
.
Akifungua mafunzo hayo jana Machi 30,2026, Mhandisi Kalimbaga, alisisitiza kuwa hatua hiyo ni ya kimkakati ya kuleta mageuzi ya kisasa katika usimamizi wa rasilimali za barabara nchini huku lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa wa pamoja juu ya mwongozo mpya na kuhakikisha uwepo wa mfumo mmoja, thabiti na ulioboreshwa wa ukusanyaji wa taarifa sahihi na za kuaminika.
.
Ambapo taarifa hizo zitawezesha upangaji na uainishaji wa vipaumbele pamoja na utekelezaji wa miradi ya barabara kwa ufanisi.
.
Mhandisi Kalimbaga alieleza kuwa kwa muda mrefu kumekuwepo na changamoto mifumo ya ukusanyaji wa taarifa kati ya TARURA na TANROADS kutowiana, hali iliyokuwa ikisababisha ukosefu wa taswira jumuishi ya mtandao wa barabara nchini.
.
“Bila takwimu sahihi, za kuaminika na zinazokidhi viwango, haiwezekani kufanya maamuzi yenye tija katika uwekezaji na matengenezo ya miundombinu ya barabara,”alisisitiza Mhandisi Kalimbaga.
.
Sanjari na hayo, alisema mwongozo wa awali ulikuwa hauendani na mahitaji ya sasa ya kimataifa katika usimamizi wa rasilimali za barabara, jambo lililosababisha kupungua kwa ubora wa taarifa.
.
Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Ujenzi kupitia Bodi ya Mfuko wa Barabara, ilichukua hatua mahsusi ya kuandaa mwongozo mpya ulioboreshwa, utakaounganishwa kikamilifu na mifumo ya kisasa ya usimamizi wa rasilimali za barabara (Road Assets Management Systems – RAMS).
.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Mhandisi Jacob Mukasa, alisema kuwa tayari hatua za awali zimeanza kuzaa matunda, ambapo takwimu za msingi kuhusu barabara, madaraja na miundombinu mingine zimekusanywa katika baadhi ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kama sehemu ya majaribio ya mfumo huo mpya.
.
Aliwahimiza washiriki wa mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kujenga uwezo wao wa kitaalamu ili kuhakikisha ukusanyaji na usimamizi wa taarifa unafanyika kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na kwa ufanisi unaotakiwa.
.
Mafunzo hayo ya siku nne, ikiwa ni awamu ya pili kwa wataalamu wa TARURA na TANROADS, yanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya barabara kwa kuimarisha matumizi ya rasilimali na kuwezesha maamuzi yanayotegemea taarifa sahihi na za kisasa.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

