logo

MOI YAZINDUA HUDUMA 9 MPYA ZA KIBOBEZI TANZANIA

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema taasisi hiyo imeendelea kupiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za kibingwa na kibobezi nchini kupitia uwekezaji wa teknolojia za kisasa pamoja na miradi ya maendeleo inayolenga kuongeza ubora wa huduma za afya.

‎.

‎Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 2, 2026 katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mtumba jijini Dodoma, Dkt. Ulisubisya amesema MOI imeanzisha huduma mbalimbali mpya ikiwemo upasuaji wa ubongo kwa kutumia akili unde (AI), upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu, huduma za uchukuaji sampuli kwa njia ya matundu pamoja na tiba ya kuweka simenti maalum kwenye pingili za mgongo zilizovunjika.

‎.

‎"Katika mwaka 2025 pekee, MOI imefanikiwa kuanzisha huduma mpya tisa za kibobezi ambazo awali zilikuwa zinapatikana nje ya Tanzania, hatua iliyopunguza gharama kubwa kwa wagonjwa waliokuwa wakisafirishwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

‎.

‎"Huduma nyingine zilizoanzishwa ni pamoja na tiba ya maumivu sugu, upasuaji rekebishi kwa viungo vilivyopooza, upasuaji wa uvimbe wa ubongo kwa kutumia teknolojia ya fluorescein pamoja na kuanzishwa kwa wodi maalum za kisasa za Premier kwa wagonjwa binafsi na wa kimataifa" alisema Dkt. Ulisubisya.

‎.

‎Aidha, amesema taasisi hiyo imeanzisha mfumo wa kisasa wa kuweka miadi kwa njia ya mtandao ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa.

‎.

‎"Katika kipindi cha mwaka mmoja, MOI imetoa huduma za kibobezi kwa wagonjwa 2,228, hatua iliyochangia kuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kuwapeleka wagonjwa kupata matibabu nje ya nchi" alisema Dkt. Ulisubisya.

‎.

‎Sambamba na hilo, MOI inaendelea na ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) lenye thamani ya shilingi bilioni 13.8, ambalo likikamilika linatarajiwa kuhudumia zaidi ya wagonjwa 1,500 kwa siku na kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano uliopo sasa.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn