MHANDISI KALIMBAGA AANZA RASMI MAJUKUMU YA URAIS WA ARMFA 2026–2027
Mhandisi Rashid S. Kalimbaga ameanza rasmi majukumu yake kama Rais wa Kamati Tendaji ya Chama cha Mfuko wa Matengenezo ya Barabara Afrika (ARMFA) kwa muhula wa mwaka 2026–2027, katika hafla ya makabidhiano, kuapishwa na kutunukiwa madaraka hayo.
Hafla hiyo muhimu ilihudhuriwa na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega (MB), pamoja na viongozi mbalimbali kutoka nchi wanachama barani Afrika.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa madaraka, Eng. Kalimbaga amemshukuru Rais anayemaliza muda wake, Eng. Moussa Essaie Aubin, kwa uongozi wake uliosaidia kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama, kujenga uwezo wa taasisi na kuinua hadhi ya ARMFA katika ngazi ya kikanda na bara zima.
Aidha, Eng. Kalimbaga amesisitiza umuhimu wa ARMFA katika kuhakikisha uendelevu wa miundombinu ya barabara barani Afrika, akitaja changamoto za kuongezeka kwa mahitaji ya matengenezo, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na changamoto za ufadhili.
.
Ametoa wito wa mshikamano, ubunifu na ushirikiano zaidi kati ya nchi wanachama kwa kuzingatia Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063 na malengo ya AfCFTA.
Katika hatua nyingine, Rais huyo ametangaza rasmi kuwa Mkutano Mkuu wa ARMFA wa mwaka 2026 utafanyika mjini Kigali, Rwanda, jambo linaloonesha mchango unaokua wa Afrika Mashariki katika ujumuishaji wa bara na usimamizi wa miundombinu.
Eng. Kalimbaga alihitimisha kwa kuahidi kutoa uongozi unaozingatia maadili, uwajibikaji na matokeo chanya, akieleza dhamira ya kuufanya muhula wake kuwa chachu ya mageuzi ndani ya ARMFA.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

