SERIKALI YATIMIZA AJIRA 12,000 NDANI YA SIKU 100
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Serikali imetekeleza kikamilifu ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuajiri vijana 12,000 ndani ya siku 100 za kwanza za kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Sita.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 30, 2026 katika Ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dodoma, Mhe. Kikwete amesema ajira hizo zinahusisha vijana 5,000 waliopangiwa sekta ya Afya na watumishi 7,000 wa sekta ya Elimu wakiwemo walimu wa Masomo ya Sayansi na Hisabati.
Alisema hadi kufikia Januari 20, 2026 waajiriwa wote walishapatikana, kupangiwa vituo vya kazi na barua za ajira zilitumwa moja kwa moja kwenye akaunti zao za waombaji, huku wengi wao wakiwa tayari wameripoti katika vituo walivyopangiwa.
“Mfumo wa ajira sasa ni wa kidijiti; waajiriwa wapya wamepokea barua zao za kazi kupitia simu za mkononi na wale waliowahi kuripoti kabla ya taarifa za mishahara kufungwa tayari wamepokea mshahara wao wa kwanza mwezi huu wa Januari,” alisema Kikwete.
Aidha, amewataka waajiriwa wapya ambao bado hawajaripoti katika vituo vyao kufanya hivyo ndani ya siku 14 tangu walipopokea barua za ajira, akionya kuwa kushindwa kufanya hivyo kutasababisha nafasi zao kuchukuliwa na waombaji wengine waliopo kwenye kanzidata ya Sekretarieti ya Ajira.
Vilevile, amewahimiza vijana wenye sifa kuendelea kuomba nafasi za ajira zitakapotangazwa, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa ajira kulingana na mahitaji ya sekta mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amesema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeboresha Mfumo wa Kielektroniki wa e-Mrejesho ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali watu katika Utumishi wa Umma.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

