logo

MCHANGO WA MADINI GDP ‎WAFIKIA ASILIMIA 12-WAZIRI MAVUNDE ‎

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa (GDP) umeongezeka kutoka asilimia 10.1 hadi kufikia asilimia 12 ndani ya siku 100 za uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mavunde ameyasema hayo leo Januari 26, 2025, wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais na mafanikio ya Serikali ndani ya siku 100, katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

‎Amesema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Taifa la Takwimu (NBS), kabla ya mwaka wa malengo 2025 mchango wa sekta ya madini ulikuwa asilimia 10.1, lakini umeendelea kuimarika kutokana na jitihada za Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji na usimamizi wa sekta hiyo.

‎Aidha, Waziri Mavunde amesema Serikali inatarajia kusaini mikataba mikubwa na kampuni za madini mapema mwezi Februari 2026 kwa ajili ya uchimbaji wa madini mbalimbali, ikiwemo madini ya niobium katika bonde la Songwe Panda Hill mkoani Mbeya.

‎Amefafanua kuwa mradi huo hautahusisha uchimbaji pekee, bali pia ujenzi wa kiwanda cha kusafisha na kuongeza thamani ya madini ya niobium kitakachozalisha Ferro-Niobium, hatua inayolenga kuongeza mapato na ajira nchini.

‎Kuhusu utafiti wa jiolojia, Mavunde amesema hadi sasa asilimia 97 ya eneo la nchi imefanyiwa utafiti wa msingi wa jiolojia, asilimia 100 utafiti wa kimagnetiki na asilimia 24 utafiti wa jiokemia.

‎Amesema lengo la Serikali ni kuongeza utafiti wa jiokemia hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, kulingana na dira ya sekta ya madini inayosema “Madini ni Maisha na Utajiri.”

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn