MIRADI YA MAENDELEO YALETA MAGEUZI MABATINI NDANI YA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA
Wakazi wa kata ya Mabatini mkoani Mwanza wamepongeza utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika eneo lao, wakisema imeleta maboresho makubwa ya kiuchumi na kijamii ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa daraja la Mabatini pamoja na uwekaji wa taa za barabarani, ambayo imesaidia kupunguza athari za mafuriko, kuimarisha usalama na kurahisisha shughuli za usafiri na biashara.
Akizungumza jana katika mahojiano maalum, mkazi wa Mabatini, Nyakasama Makore, alisema ujenzi wa daraja hilo pamoja na taa za barabarani umewezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi hadi nyakati za usiku.
“Taa za barabarani zimetupa usalama na sasa wafanyabiashara wanaweza kufanya kazi hadi usiku bila hofu,” alisema Makore.
Kwa upande wake, msimamizi wa mradi wa Mabatini kutoka kampuni ya Nyanza Road Works, Kulwa Chigugu, alisema uboreshaji wa miundombinu umeongeza usalama, kurahisisha usafiri na kusaidia wananchi hususan vijana kupata ajira na kipato.
Alisema kupitia utekelezaji wa mradi huo, wafanyakazi zaidi ya 60 wameajiriwa, hali iliyosaidia kuongeza kipato kwa familia nyingi katika eneo hilo.
Naye mkazi mwingine wa Mabatini, Mariam Samweli, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapelekea mradi wa taa za barabarani, akisema umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya uhalifu na kuongeza fursa za shughuli za kiuchumi.
Aliongeza kuwa wananchi wanaendelea kushirikiana na Serikali katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kampeni za usafi wa mazingira, huku wakionesha matumaini ya kuendelea kunufaika na miradi mingine ya maendeleo.
Wakati huo huo, utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja na barabara katika kata ya Mkuyuni unaendelea vizuri, huku mkandarasi akiendelea na kazi za mwisho za umaliziaji.
Kwa mujibu wa msimamizi wa mradi huo, Sefrosa Lyatuu, mkandarasi wa mradi, Jasco Company, kwa sasa anaendelea na ujenzi wa mitaro na tayari ameshaweka taa za barabarani katika baadhi ya maeneo ya mradi.
Alisema kabla ya ujenzi wa daraja hilo, eneo la Mkuyuni lilikuwa likikumbwa na mafuriko hasa katika kipindi cha masika, hali iliyokuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.
“Kwa sasa mradi umefikia asilimia 99 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni,” alisema Lyatuu.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Charles Ndelema, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea wananchi mradi huo muhimu, akisema umeongeza fursa za ajira na kurahisisha maisha ya wananchi.
Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa Mabatini na Mkuyuni.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

