BIMA YA AFYA KWA WOTE UTEKELEZAJI WAKE KUANZA RASMI JANUARI 26
Serikali imetangaza kuanza rasmi utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote (UHC) awamu ya kwanza, itakayowanufaisha wananchi wasio na uwezo wakiwemo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu, ambapo gharama zao zitagharamiwa na Serikali.
Aidha, Serikali imetangaza kitita cha huduma muhimu kitakachotolewa kupitia skimu za Bima ya Afya kwa gharama ya Shilingi 150,000 kwa kaya yenye watu wasiopungua sita.
Akizungumza leo Januari 23, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utaanza rasmi Januari 26, 2026, akisisitiza umuhimu wa watendaji kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kujiunga na mpango huo.
Waziri Mchengerwa amesema kwa ada hiyo ya Shilingi 150,000, kaya moja itahusisha mwanachama mchangiaji, mwenza wa mwanachama pamoja na wategemezi wanne.
Amefafanua kuwa wategemezi hao wanaweza kuwa mzazi wa mwanachama au wa mwenza wake, mtoto wa kuzaa, kuasili au wa kambo mwenye umri chini ya miaka 21, pamoja na ndugu wa damu aliye chini ya umri huo.
Ameongeza kuwa huduma zitakazotolewa zitazingatia mfumo wa rufaa katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoingia mkataba na skimu za Bima ya Afya.
Waziri Mchengerwa amewataka viongozi na watendaji kuhakikisha elimu sahihi inawafikia wananchi ili kutimiza lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kwa uhakika kupitia Bima ya Afya kwa Wote.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

