JKT YATANGAZA MAFUNZO YA KUJITOLEA KWA MWAKA 2026
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele, amewaarifu vijana wote wa Tanzania Bara na Visiwani kujitokeza kuomba kujiunga na Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa kujitolea kwa mwaka 2026.
Amesema mchakato wa kuomba na kuchaguliwa kujiunga na mafunzo hayo unasimamiwa na kuratibiwa kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya kulingana na makazi ya mwombaji.
.
Hayo yameelezwa leo Januari 20, 2026 jijini Dodoma na Mkuu wa Tawi la Utawala Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
.
"Vijana wenye taaluma za TEHAMA ikiwemo Diploma na Shahada katika fani za Information Technology, Business Information Systems, Computer Science, ICT, Cyber Security and Digital Forensics, Computer Engineering, Computer Networks and Information Security Engineering pamoja na vijana wenye vipaji mbalimbali vya michezo, wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kupitia mikoa yote.
"Usaili wa kuwapata vijana watakaojiunga na Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa kujitolea utaanza rasmi tarehe 26 Januari 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani" alisema Brigedia Jenerali Mabena.
Aidha, Amesema Vijana watakaoteuliwa watatakiwa kuripoti kwenye makambi ya JKT kuanzia tarehe 27 Februari 2026 hadi tarehe 04 Machi 2026.
Hata hivyo, JKT imefafanua kuwa haitoi ajira wala haina jukumu la kuwatafutia ajira wahitimu wake katika asasi, vyombo vya ulinzi na usalama, au taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, badala yake, mafunzo yanayotolewa yanalenga kuwawezesha vijana kujiajiri na kujitegemea baada ya kukamilisha mkataba wao.
Sifa za waombaji pamoja na maelekezo ya vifaa vinavyotakiwa kwa washiriki wa mafunzo hayo vinapatikana kupitia Tovuti rasmi ya JKT ambayo ni www.jkt.mil.tz.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

