BARABARA YA KIGOMA-TABORA KILOMITA 413 YAKAMILIKA KWA KIWANGO CHA LAMI
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya ameupongeza Wakala wa Barabara nchini TANROADS mkoa wa Kigoma kwa kumsimamia vizuri mkandarasi STECOL Cooperation Ltd, anaejenga barabara ya Malagarasi-Ilunde- Uvinza km 51.1 kwa kuikamilisha kwa viwango.
Kukamilika kwa barabara hiyo sasa kunaifanya barabara yote ya Tabora-Kigoma km 413 kukamilika kwa kiwango cha lami.
Akizungumza wakati akikagua barabara hiyo Eng. Kasekenya amemtaka mkandarasi STECOL anaejenga barabara hiyo kukamilisha daraja la Ruchugi katika kipindi cha mwezi mmoja toka sasa ili barabara hiyo lianze kutumika.
“Kukamilika kwa sehemu hii sasa kunaifanya barabara yote toka Tabora hadi Kigoma km 413 kuwa ya lami na kuandika historia mpya kwa mikoa ya magharibi na Tanzania kwa ujumla”, amesema Eng. Kasekenya.
Amesema Serikali imedhamiria kuufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara za lami kila upande, usafiri wa anga, reli na meli ili kuufanya mkoa huo kitovu cha uchumi wa mikoa ya magharibi na nchi jirani za Burundi na DRC.
Amesema barabara unganishi za Uvinza- Kasulu na Uvinza-Mishamo-Mpanda ziko katika hatua mbalimbali za maandalizi ya ujenzi wake.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipanga kuufungua ukanda wa magharibi mwa nchi kimiundombinu ili kukuza uchumi”, amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani ameishukuru Serikali kwa uwekezaji wa miundombinu ya kisasa mkoani Kigoma ambayo inachochea fursa za kilimo, biashara na uvuvi na hivyo kukuza uchumi.
Meneja wa TANROADS mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa wamejipanga kuhakikisha daraja la Ruchugi na mzunguko wa Uvinza vinakamilishwa kabla ya mwisho wa mwezi Februari.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

