PROF.KUSILUKA:AKILI UNDE HAIKWEPEKI, ELIMU LAZIMA IENDANE NA KASI YA TEKNOLOJIA
Wanataaluma na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) leo Desemba 16, 2025 wamekutana jijini Dodoma katika Kongamano la 16 la kitaaluma, kwa lengo la kujadili kwa kina mchango na athari chanya za matumizi ya teknolojia ya kisasa, hususan Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), katika kukuza elimu, utafiti na maendeleo ya jamii.
Kongamano hilo limewakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali za elimu na teknolojia, na limeelezwa kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana maarifa na uzoefu kuhusu namna teknolojia za kidijitali zinavyoweza kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi kazini pamoja na kuibua fursa mpya za ajira, hususan kwa vijana.
Akizungumza mara baada ya kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Lughano Kusiluka, amesema Akili Unde ni teknolojia isiyokwepeka katika dunia ya sasa, hivyo ni muhimu kuhakikisha inatumika kwa namna yenye kuleta tija na maendeleo chanya.
Profesa Kusiluka amesema vijana wa Kitanzania wanaonesha uwezo mkubwa katika masuala ya teknolojia za kidijitali, huku akieleza kuwa UDOM ni miongoni mwa taasisi zinazoongoza nchini katika kuzalisha wahitimu mahiri kwenye nyanja hizo.
Ameongeza kuwa dhamira ya chuo hicho ni kuhakikisha Watanzania hawaachwi nyuma katika mapinduzi ya teknolojia yanayoendelea duniani, akibainisha kuwa matumizi sahihi ya Akili Unde yamechangia kwa kiasi kikubwa kuharakisha maendeleo katika maeneo mbalimbali.
Aidha, Profesa Kusiluka ameeleza kuwa kutokana na kuenea kwa matumizi ya Akili Unde, UDOM imekuwa ikiboresha mifumo ya mitihani kwa lengo la kumpima mwanafunzi mwenyewe, na si teknolojia.
“Tunazingatia aina ya mitihani inayohakikisha tunamtathmini mwanafunzi halisi, kwa sababu matumizi mabaya ya teknolojia yanaweza kuathiri ubora wa wahitimu. Ndiyo maana tunatumia mbinu mbalimbali ikiwemo mitihani ya vitendo, ambako Akili Unde haiwezi kujibu kwa niaba ya mwanafunzi,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Gilead Teri, amesema Chuo Kikuu cha Dodoma kimeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuzalisha viongozi, wajasiriamali, wafanyabiashara na watumishi wa umma wenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Amesisitiza umuhimu wa kuwa na akili mtambuka, akieleza kuwa elimu peke yake haitoshi bila kuambatanishwa na ujuzi wa ziada na matumizi ya teknolojia katika shughuli za kila siku, jambo ambalo linaongeza tija na matokeo chanya katika maeneo ya kazi.
Kwa upande wao, wahitimu wa UDOM walioshiriki kongamano hilo wamesema mjadala huo umewapa mwanga na motisha ya kukabiliana na kasi ya ukuaji wa teknolojia, huku wakieleza kuwa utawasaidia kujitayarisha vyema kwa soko la ajira.
Kongamano la 16 la wanataaluma na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma limehitimishwa kwa wito kwa taasisi za elimu ya juu nchini kuwekeza zaidi katika teknolojia za kisasa, hususan Akili Unde, ili kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya dunia ya sasa na ya baadaye.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

