TCRA-CCC YATAKIWA KUONGEZA USHIRIKIANO NA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA MAWASILIANO
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amefanya ziara ya kikazi katika Baraza la Ushauri wa Mawasiliano Tanzania (TCRA Consumers Consultative Council – TCRA CCC) leo tarehe 08 Disemba 2025, jijini Dar es Salaam, ili kujionea namna Baraza linavyotekeleza majukumu yake ya kulinda haki na maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini.
Katika maelezo yake kwa uongozi wa Baraza hilo, Waziri Kairuki aliwataka kuendelea kufuatilia kwa ukaribu mchakato wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi, na kuonesha wazi aina ya malalamiko yaliyoshughulikiwa na yale yanayoendelea kufanyiwa kazi.
.
Alisisitiza kuwa ni muhimu Baraza likajiimarisha ili kutatua malalamiko yanayotolewa na watumiaji wa huduma za Mawasiliano.
Mhe. Kairuki pia aliagiza Baraza hilo kuendeleza ushirikiano na wadau wake pamoja na watumiaji wengine wa huduma wakiwemo watoa huduma za mawasiliano na makundi maalum ya wananchi, ili kuhakikisha changamoto zao zinapewa kipaumbele na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Aidha, Waziri Kairuki amelitaka baraza hilo kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu haki zao na matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano ili kuimarisha uelewa na kuongeza uwajibikaji wa watoa huduma.
Akihitimisha ziara hiyo, Mhe. Kairuki alisema Baraza la Ushauri wa Mawasiliano ni chombo muhimu sana katika sekta ya mawasiliano, kwa kuwa linatoa mchango mkubwa katika kulinda haki za wananchi, hususan wale wenye mahitaji maalum, ili nao waweze kunufaika ipasavyo na huduma za mawasiliano nchini.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

