logo

ULEGA ATOA MIEZI 2 KWA SHANDONG KUKAMILISHA BARABARA YA MWENGE HADI TEGETA

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa miezi miwili kwa kampuni ya Shandong Luqiao Group kukamilisha ujenzi wa barabara ya MwengeTegeta kama mkataba unavyosema la sivyo serikali itauvunja na kutafuta mkandarasi mwingine.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miundombinu ya barabara na madaraja jijini Dar es Salaam, Ulega alisema muda wa mkataba wa ujenzi huo uliisha tangu Septemba mwaka huu na kwamba muda huo wa miezi miwili ni nafasi yake ya mwisho kuonyesha uwezo wake wa kazi.

“Niliwahi kuja kuutazama mradi huu uko nyuma na nikaambiwa muda wake mwisho ni Septemba. Tukatumia busara kusema tuwaongeze walau miezi mitatu wamalize, lakini naona tukiwapa mgongo wanaendelea na mambo yao mengine. Sasa natoa miezi miwili ya mwisho, wakishindwa tutavunja mkataba na kutangaza zabuni upya ili kumpata mkandarasi mwenye uwezo wa kukamilisha mradi huo” amefafanua Ulega.

Ulega amesema mkandarasi wa kampuni hiyo ya Shandong imekuwa ikionesha uzembe na kutozingatia maelekezo ya Serikali licha ya kupewa muda wa kutosha kukamilisha mradi huo unaogusa maisha ya Watanzania moja kwa moja.

Amesisitiza Serikali haitavumilia mkandarasi yeyote anayeshindwa kutekeleza kazi zake kwa uadilifu, nidhamu na kasi inayostahili, hasa kwa miradi yenye umuhimu kama barabara zinazoelekea maeneo ya makazi na biashara.

Waziri huyo amesema kuwa Serikali ina dhamira ya kuhakikisha miradi yote ya miundombinu ya barabara inakamilika kwa wakati ili fedha za wananchi zitumike kwa tija na kuleta matokeo yanayoonekana.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn