BMH YAADHIMISHA SIKU YA USALAMA WA MGONJWA DUNIANI
Kila ifikapo Septemba 17 kila mwaka dunia huadhimisha siku ya usalama wa mgonjwa duniani na mwaka huu siku hii imeangazia usalama wa watoto wachanga maeneo ya kutolea huduma za afya.
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ni miongoni mwa taasisi za afya nchini zinazozingatia usalama wa mtoto pindi anapopata huduma na mwaka huu wameadhimisha siku hii kwa kutoa msaada kwa watoto wachanga waliozaliwa kabla ya muda na wale wenye changamoto zingine za kiafya.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Henry Humba kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Prof Makubi , amesema kuwa BMH inafuata miongozo iliyowekwa na wizara ya afya kuhusiana na masuala ya usalama wa mgonjwa awapo eneo la kupata huduma za afya.
"BMH kama taasisi ya afya inafuata miongozo yote iliyowekwa na wizara ya afya kwenye masuala ya usalama wa wagonjwa na hususani watoto wachanga ndio maana hospitali imewekeza kusomesha madaktari bingwa kwenye maeneo ya ubobezi wa magonjwa ya watoto, miundombinu na vifaa tiba lengo letu ni kuwa mtoto anapoingia hospitali akiwa mgonjwa atoke akiwa amepona kabisa," amesema Dkt. Humba.
Dkt. Humba ameendelea kwa kusema kuwa dhana ya usalama kwa wagonjwa ni pana na kila mtu anasehemu yake ndio maana hata serikali imeweka mipango mbalimbali ya kuhakikisha usalama wa watoto ikipewemo sera ya afya inayoongelea vipaumbele mbalimbali ikiwemo kuwatolea gharama za matibabu kundi hili.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya watoto, Emmy Mbilinyi amesema kuwa BMH imejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa mtoto pindi anapofika BMH kupata huduma.
"Hospitali yetu imejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa mtoto pindi anapokuja kupata huduma mfano katika kitengo hiki cha uangalizi maalum wa watoto wazazi na watoa huduma hawaruhusiwi kuingia na nguo zao za nyumbani kwani wanaweza kusababisha maambukizi kwa watoto na pia ni lazima kunawa mikono kabla ya kuanza kuhudumia mtoto hii yote ni kuhakikisha mtoto anakuwa salama," amesema Dkt. Emmy.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

