MAJALIWA AZINDUA KAMPENI ZA UBUNGE JIMBO LA MCHINGA
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Septemba 07, 2025 amezindua kampeni za Ubunge jimbo la Mchinga zilizofanyika katika kijiji cha Rutamba mkoani Lindi
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030 imejielekeza katika kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kote nchini ikiwemo katika jimbo la Mchinga.
“Katika kipindi kilichoisha Rais Dkt. Samia ameleta hapa miradi mikubwa, ya kati na midogo, anafanya hivi kwa kutambua wananchi wanapaswa kuhudumia, hata ilani hii imeonesha maeneo mengine yatakayotekelezwa katika mkoa huu wa Lindi”
Amesema kuwa Wana-Lindi wanapaswa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kutekeleza miradi ya gesi, bandari ya uvuvi Kilwa, ujenzi upya wa barabara ya Dar-Lindi, maboresho ya uwanja wa ndege wa Lindi, ujenzi wa reli ya kanda ya kusini pamoja na kuunganisha mkoa wa Lindi kwenye gridi ya Taifa ili kuwa na umeme wa uhakika.
Amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameleta mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wa Lindi, ilani hii imeendelea kusheheni miradi inayokwenda kutekelezwa katika maeneo yetu, hii ni sababu pekee ya sisi kumchagua Rais Dkt. Samia.
“Ilani ya uchaguzi ya 2025/2030 imeonesha kuwa kutaanza kujengwa kwa kiwango cha lami barabara ya Ngongo-Ng’apa, Mandawa hadi Chikundi, barabara hii itakuwa ni mkombozi kwa wakati wa wakazi wa maeneo haya na itafungua uchumi kwa Wana-Lindi.” alisema Majaliwa.
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Jimbo hilo limefanikiwa kuwa na magari ya wagonjwa Manne pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na zahanati ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuboresha huduma za afya katika jimbo hilo.
“Mheshimiwa Salma Kikwete amejikita katika kuwahudumia wananchi, kwa namna jimbo hili lilivyokaa linahitaji mtu mahiri na mwenye dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wake, hakika Mheshimiwa Salma ameonesha ameweza, mchagueni tena” alisema.
Kwa Upande wake mgombea ubunge wa jimbo hilo Bi. Salma Kikwete amesema kuwa katika katika kipindi chake amefanikiwa kushirikiana na WanaMchinga kutafuta majibu ya changamoto yaliyo katika jimbo hilo
“Tumepata mafanikio makubwa katika kukabiliana na changamoto zetu, hali ilivyo leo sio sawa na tulikotoka, tumepata mafaniko katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, nishati, elimu, maji, miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi, nikipata ridhaa tena tutafanya makubwa zaidi” alisema Salma Kikwete.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

