WATANZANIA MILIONI MOJA WAPEWA MATIBABU BURE KWENYE SOBER HOUSE-CG LYIMO
SERIKALI ya Awamu ya Sita kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kumtibu bure rapa wa muziki wa Hip Hop nchini Rashidi Abdallah Mohamed Makwiro maarufu Chid Benz ambaye kwa miaka kadhaa alitumbukia kwenye uraibu wa dawa za kulevya, hivyo kudhoofika kiafya na kushindwa kutekeleza majukumu yake.
.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema,Chid Benz ni miongoni mwa Watanzania milioni moja ambao wamepatiwa matibabu bure kutokana na uraibu wa dawa za kulevya kote nchini.
.
Ameyasema hayo leo Agosti 22,2025 katika ofisi za DCEA jijini Dar es Salaam wakati akimkabidhi Chid Benz kwa familia na Watanzania baada ya Serikali kumpatia matibabu yaliyodumu ndani ya mwaka mmoja.
.
Ameeleza kuwa DCEA licha ya majukumu iliyokasimiwa na Serikali ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini, pia imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kunakuwa na ustawi bora wa jamii nchini.
.
"Lakini, jukumu letu lingine ni kuhakikisha kwamba tunajenga ustawi wa jamii ili wale ambao wamekwishajingiza katika matumizi ya dawa za kulevya tunahakikisha kwamba, tunawaondoa kwenye hayo matumizi ya dawa za kulevya." alisema Lyimo.
.
Amesema kuwa, mafanikio hayo ya kumpatia Chid Benz na watu wengine matibabu yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ikiwemo miundombinu kwa mamlaka hiyo ili kuhakikisha wale ambao wameathiriwa na dawa za kulevya hususani vijana wanawapatia matibabu nchini.
.
Aidha, Kamishna Jenerali amesema, kutokana na Chid Benz kutokuwa na uelewa kuhusu athari za dawa tiba hizo ambazo zinatumika kwa uangalizi maalum kutibu saratani na kufanyiwa upasuaji, zilimuathiri zaidi kiafya.
.
Kutokana na madhara hayo, Serikali ilimchukua Chid Benz na kumpeleka katika kituo cha upataji nafuu cha Pili Missana Foundation kilichopo jijini Dar es Salaam na sasa amepona.
.
Ameongeza kuwa, kati watu hao milioni ambao kwa nyakati tofauti wamepatiwa matibabu bure na Serikali kote nchini wengi wao ni vijana.
.
"Tunamtoa Chid Benz kama mfano wa vijana ambao wamepatiwa tiba na Serikali na wanerudi katika hali yao ya kawaida, kwa wanaomzoea Chid Benz kabla ya kupata matibabu na kuchukuliwa na Serikali hali yake ilikuwa mbaya sana na walimzushia kifo."
Amesema, baada ya Serikali kumpatia matibabu sasa afya yake imeimarika na yupo tayari kuanza kuwahudumia wananchi kwa burudani kama zamani na kuhakikisha nchi inaendelea kufurahi kwa kuwa na mwanamuziki hodari.
Chid Benz.
.
Kwa upande wake, Chid Benz ameishukuru DCEA kwa kumuonesha moyo wa upendo, kwani awali alikata tamaa baada ya kuathiriwa na matumizi ya heroin na dawa tiba zenye asili ya kulevya, lakini sasa yupo imara.
.
"Kwa kawaida watu husema bahati haiji mara mbili, sasa hivi nipo sawa na karibuni nitarudi mtaani kuendelea na kazi zangu, ninaombeni ushirikiano wenu, ninaishukuru sana mamlaka, ninamshukuru Brother Lyimo (Kamishna Jenerali Lyimo) kwa kunisaidia, Dkt.Mapana nipo bega kwa bega nao na nitafanya kazi kwa bidii."
.
Aidha, Chid Benz ametoa angalizo kwa wasanii wenzake kuepuka matumizi ya dawa za kulevya kwani si tu kwamba zinaathiri afya, bali pia zinaua ndoto na kipaji.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

