TANZANIA TUMEIVA TUNAENDA KUKOMESHA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA-WAZIRI MKUU MAJALIWA
WAZIRI MKUU Mhe. Kassim Majaliwa ametoa onyo kwa wasambazaji na wauzaji wa dawa za kulevya kwamba Tanzania siyo mahali pa kufanyia biashara zao.
Waziri Mkuu ambaye amefunga maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema:
“Tanzania siyo mahali salama kwa wauzaji, wasafirishaji na walimaji na hata pia watumiaji wa dawa za kulevya. Tanzania tumeiva na sasa tunaenda kukomesha biashara hii.”
Mhe. Majaliwa ametoa kauli hiyo leo jioni (Alhamisi, Juni 26, 2025) wakati akizungumza na maelfu ya wakazi wa Dodoma wakiwemo wananchi, wadau, viongozi wa Serikali, wa dini na siasa ambao walihudhuria kilele cha maadhimisho hayo kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
“Makamishna na wakuu wa vyombo vya ulinzi fanyeni kazi, imarisheni ulinzi iwe ni kwenye SGR, vituo vya mabasi, bandari na viwanja vya ndege ili tuweze kuokoa vijana wetu. Dawa hizi zina madhara makubwa kwani zinapoteza uwezo wa mwili na uwezo wa kiakili wa kufikiri mambo,” amesisitiza.
Amesema kuwa anatambua kwamba kuna mjadala ulioibuka baina ya wachumi na wadau wa kuzuia matumizi ya dawa za kulevya huku wachumi wakidai kuwa zinaleta fedha na kuacha kuangalia madhara ya kiafya ambayo wadau wanayasemea.
.
“Kama tunataka tuwe na kundi la vijana wa Kitanzania mazezeta, basi turuhusu hii biashara. Lakini, Serikali hii tumekataa kwa sababu tunaamini kuwa hiyo mijadala haina tija na hatutairuhusu,” alisema.
.
Naye Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema kutokana na uongozi madhubuti wa Serikali ya awamu ya sita, kwa kipindi cha kuanzia Juni, 2024 hadi Mei, 2025, kumekuwa na ongezeko la ukamataji wa dawa za kulevya ukilinganisha na miaka iliyopita.
“Katika kipindi hiki, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, tumekamata dawa za kulevya jumla ya kilogramu 2,301,414.94. Kiasi hiki ni kikubwa ikilingalishwa na kilo 2,050,542.73 zilizokamatwa kati ya Juni, 2023 na Mei, 2024.
.
"Kuanzia Januari hadi Desemba 2024, jumla ya kilo 2,327,983.8 zilikamatwa ikilinganishwa na kilo 1,965,341 zilizokamatwa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2023.” alisema Lyimo.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

