WIZARA YA ARDHI YAFANIKIWA KUKAMILISHA MAREKEBISHO YA SERA YA TAIFA YA ARDHI YA MWAKA 1995
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amesema katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, Wizara hiyo imefanikiwa kukamilisha marekebisho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 na hivyo kuwa na Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 (Toleo la mwaka 2023) na tayari imezinduliwa tarehe 17 Machi 2025 na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
.
"Malengo makuu ya Sera hiyo ni kuhakikisha kuna mfumo madhubuti wa umiliki wa ardhi, usawa katika upatikanaji ardhi, usimamizi na matumizi ya ardhi kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii" alisema Ndejembi.
.
Waziri Ndejembi ameyasema hayo leo Mei 23,2025 Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
.
Amesema idadi ya mipango ya matumizi ya ardhi imeongezeka kutoka vijiji 2,088 hadi vijiji 4,679 ikiwa ni ongezeko la viijiji 2,591 sawa na asilimia 124.
.
"Ongezeko hilo limesababishwa na jitihada za Serikali za kuhakikisha kuwa vijiji vyote nchini vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi pamoja na mwitikio wa wadau katika kuchangia uandaaji wa mipango hiyo" alisema Ndejembi.
.
Kwa upande mwingine, Waziri Ndejembi amesema Wizara imeandaa programu maalum ya uendelezaji upya maeneo yaliyochakaa katika miji mbalimbali nchini. Programu hii itasaidia kuboresha huduma za msingi katika maeneo hayo na hivyo kuyawezesha kuchangia ipasavyo katika Pato la Taifa.
.
"Programu hii imelenga kuboresha maisha ya wakazi, kupunguza umaskini, kuongeza fursa za kiuchumi na kuhakikisha miji inakuwa endelevu na inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa na majengo, miundombinu na huduma bora zaidi kwa Watanzania.
.
"Kupitia Programu hii, jumla ya maeneo 111 yenye ukubwa wa hekta 24,309.349 yameainishwa katika mikoa 24 kwa ajili ya kupangwa na kuendelezwa upya ili kuwa na tija kiuchumi na kijamii" alisema Waziri Ndejembi.
.
Aidha, Waziri Ndejembi amesema Wizara imepokea shilingi bilioni 64.5 kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika Halmashauri 131 ikiwemo shilingi bilioni 50 zilizokopeshwa kwenye Halmashauri 57 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Ardhi (Plot Development Revolving Fund (PDRF). Fedha hizo zimewezesha upangaji na upimaji wa viwanja 556,191.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

