
COSOTA YASULUHISHA MIGOGORO 118 KATI YA 136
Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki (COSOTA), Bi. Doreen Sinare amesema kwa mwaka 2021-2025 COSOTA imefanikiwa kufanya migao miwili kama alivyoahidi Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipolihutubia bunge mwaka 2021 ambapo alisisitiza katika kipindi cha uongozi wake, serikali itahakikisha wabunifu wote wananufaika zaidi na kazi zao.
.
"Mgao wa kwanza ambao ulikuwa ni mgao wa ishirini na tatu ulifanyika tarehe 28/01/2022 na ulikuwa wa kiasi cha Tshs. Tshs. 312,290,259,000, ambapo wasanii 1,123 walinufaika, na ulitokana na matumizi ya kazi 5,924 za muziki ambazo zilitumika katika vituo 11 vya redio, ikiwemo redio katika ngazi ya kitaifa, Mkoa, wilaya, kijamii na za kidini.
.
"Mgao wa pili katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita ulifanyika tarehe 21/07/2023 na ulikuwa ni mgao wa ishirini na nne wa mirabaha kwa kazi za muziki na COSOTA iligawa kiasi cha Tshs. 396,947,743.20 na wasanii wa muziki 8,165 walinufaika kupitia kazi zao 61,490" alisema Bi. Doreen.
.
Bi. Doreen ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 21, 2025 jijini Dodoma.
.
Amesema hivyo ni viwango vikubwa zaidi kuwahi kufanyika katika migao ya mirabaha ambayo COSOTA imekuwa ikigawa kwa miaka ya nyuma kabla ya uongozi huu wa serikali ya awamu ya sita ambao ulianzisha kampeni ya kusisitiza watumiaji wa kazi za Sanaa katika maeneo ya biashara kulipia matumizi ya kazi hizo.
.
Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema kwa kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita COSOTA imefanikiwa kupokea jumla ya migogoro 136 na kusuluhisha migogoro 118.
.
"Migogoro 10 kati ya hiyo haikumalizika na ilifunguliwa kesi mahakamani na migogoro 8 inaendelea COSOTA. Sambamba na migogoro hii, COSOTA imehusika na kesi za hakimiliki 10" alisema.
.
Aidha, Bi. Doreen amesema Muziki wa singeli ambao ni wa kipekee kutoka Tanzania umekua kwa kasi, na kupendwa zaidi nchini na kuvuka mipaka ya nchi, katika kipindi hiki, COSOTA imetoa elimu kwa Wasanii, watayarishaji, wafanyabiashara na wadau wa Singeli ambapo takribani wasanii 20 wa Muziki wa Singeli wamesajili kazi zao COSOTA.
.
"Pia wamenufaika na mgao wa mirabaha kwa mwaka 2022 na mwaka 2023 na ni mategemeo yetu kuwa watanufaika zaidi kutokana na kupendwa na kushiriki katika biashara ya muziki wa singeli ndani nan je ya nchi" alisema.
Tranding News

Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news