WANAFUNZI 188,128 WACHAGULIWA KUJIUNGA NA KIDATO CHA 5
SERIKALI imekamilisha zoezi la Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule za Sekondari,Vyuo vya Ualimu,Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Kati vya Serikali Mwaka 2023, ambapo jumla ya wanafunzi 188,128 waliokidhi vigezo wamechaguliwa.
.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi huo Waziri Nchi,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Angellah Kairuki amesema wanafunzi hao wote wamepangiwa kujiunga na Kidato cha Tano katika shule mbalimbali nchini pamoja na Vyuo.
.
Kairuki Amesema zoezi hilo limefanyika kwa kuzingatia Takwimu za matokeo ya Wanafunzi waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2022, kutoka Tanzania Bara ambapo wanafunzi waliochaguliwa ni kutoka Shule za Serikali, zisizo za Serikali, watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.
.
Amesema matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2022 yanaonesha kuwa Watahiniwa 192,348 (36.95%) walipata ufaulu wa Daraja la I – III ambapo kati ya hao Tanzania Bara walikuwa watahiniwa 188,128 wakiwemo wasichana 84,509 na wavulana 103,619.
“Wanafunzi hao wote wamekidhi vigezo vya kujiunga na Kidato cha Tano, Vyuo vya ualimu,Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Kati kwa mwaka, 2023. Idadi hii inajumuisha Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum 490 ambao wasichana ni 218 na wavulana ni 272.” alisema Kairuki.
.
Waziri huyo Amesema Wanafunzi 129,830 wakiwemo wasichana 66,343 na wavulana 63,487 Sawa na asilimia 69 ya wenye sifa, wamechaguliwa kujiunga na Shule za Sekondari za Kidato cha Tano ambapo, Wanafunzi 1,878 wakiwemo wasichana 1,097 na wavulana 781 wamepangiwa katika Shule za sekondari Maalum za Kilakala, Mzumbe, Ilboru, Kisimiri, Msalato, Kibaha, Tabora Boys na Tabora Girls.
.
Aidha, Kairuki amesema Muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano utaanza tarehe 14 Agosti,2023 na kwamba hivyo, Wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na Kidato cha Tano kwa mwaka, 2023 wanapaswa kuanza kuripoti Shuleni kuanzia tarehe 13 Agosti, 2023 huku siku ya mwisho ya kuripoti ikitajwa kuwa ni 31 Agosti, 2023.
“Fomu za maelezo ya mahitaji ya kujiunga na Kidato cha Tano kwa Shule zote za Kidato cha Tano zinapatikana kwenye tovuti ya OR-TAMISEMI kupitia kiunganishi cha www.tamisemi.go.tz .”alisema Kairuki
#JordanMediaupdates
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

