RIBA YA BoT YABAKI ASILIMIA 5.75 ROBO YA KWANZA YA MWAKA 2026
Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kuendelea kubakiza kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kuwa asilimia 5.75 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026, sawa na kiwango kilichotumika katika robo ya nne ya mwaka 2025.
Uamuzi huo umetangazwa Januari 8, 2026 na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha, Bw. Emmanuel Tutuba, wakati wa mkutano na viongozi wa benki, taasisi za fedha pamoja na waandishi wa habari.
Akizungumza katika mkutano huo, Gavana Tutuba amesema uamuzi wa kubakiza CBR umetokana na tathmini ya kina ya mwenendo wa uchumi wa ndani na wa kimataifa, sambamba na matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.
Ameeleza kuwa kuendelea kwa kiwango hicho cha riba kutasaidia kuchochea shughuli za kiuchumi, kuimarisha upatikanaji wa mikopo na kuwezesha uchumi wa taifa kuendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha.
Kuhusu hali ya uchumi wa ndani, Gavana Tutuba amesema uchumi wa Tanzania Bara uliendelea kukua kwa wastani wa asilimia 5.9 mwaka 2025, karibu na makadirio ya asilimia 6, huku ukuaji huo ukichangiwa kwa kiasi kikubwa na sekta za kilimo, madini na ujenzi.
Kwa upande wa Zanzibar, amesema uchumi unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.8 mwaka 2026, ukichochewa zaidi na shughuli za ujenzi, utalii na uzalishaji viwandani.
Aidha, Gavana Tutuba amewapongeza wadau wa sekta ya fedha kwa juhudi zao zilizopelekea kupungua kwa uwiano wa mikopo chechefu hadi asilimia 3.1, kiwango kilicho chini ya ukomo unaokubalika wa asilimia 5.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

