logo

WAZIRI MKUU AHIMIZA WANANCHI KUFANYA UCHUNGUZI WA AFYA MARA KWA MARA

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kuchunguza afya mara kwa mara ili kufahamu hali zao za kiafya na kuchukua hatua mapema endapo atakutwa na changamoto yoyote.

Majaliwa ametoa rai hiyo leo Mei 10, 2023 katika hafla ya uzinduzi wa huduma za upandikizaji wa Uloto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.

"Nitoe rai kwa jamii ya Watanzania kujenga utamaduni wa kuchunguza afya zao mara kwa mara kwa lengo la kufahamu afya zao na kuchukua hatua mapema." Amesema Majaliwa.

Amesema kuwa, uwekezaji wa kituo hicho kinachotoa huduma ya upandikizaji wa Uloto uliofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.7 , huku huduma hizo zikisaidia kupunguza gharama kubwa iliyokuwa inatumiwa na Serikali ili kuwezesha Watanzania wenye uhitaji kupata huduma hizo nje nchi.

Aidha, Majaliwa amesema, huduma hii ya upandikizaji uloto ikitolewa ndani ya nchi katika Hospitali hii ya Benjamin Mkapa itagharimu shilingi milioni 50 hadi 55 kwa mgonjwa mmoja na kama angepelekwa nje takriban shilingi milioni 120 hadi 150 zingetumika.

Ameendelea kusisitiza kuwa, upandikizaji uloto unatoa nafuu kubwa sana kwa wagonjwa wa Seli Mundu (Sickle Cell) kwa kuwapunguzia kwa kiasi kikubwa maumivu na maambukizi ya mara kwa mara na wakati mwingine huwa sababu ya kupona kabisa kwa ugonjwa huu wa kudumu hivyo kutoa fursa ya wagonjwa hao kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa.

Sambamba na hilo,Majaliwa amesema, katika kipindi cha miaka miwili ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imeokoa shilingi bilioni 3.5 kwa kutoa huduma ya upandikizaji figo nchini.

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn