KILOGRAMU 1,965,340.52 ZA DAWA ZA KULEVYA ZILIKAMATWA MAENEO MBALIMBALI NCHINI 2023 -WAZIRI MHAGAMA
Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.Jenista Mhagama amesema kwa mwaka 2023, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) imefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 10,522 ambao kati yao wanaume ni 9,701 na wanawake ni 821 walikamatwa kuhusika na dawa hizo, na jumla ya hekari 2,924 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa.
.
"Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti Kupambana na Dawa za Kulevya imepata mafanikio makubwa ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Disemba 2023 kilogramu 1,965,340.52 za aina mbalimbali za dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini" alisema.
.
Mhagama ameyasema hayo leo February 20,2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dodoma juu ya Mafanikio ya Serikali katika Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya kwa mwaka 2023.
.
Amesema Kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja pekee ni kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa hapa nchini kwani kinazidi kiasi cha kilogramu 660,465 zilichokamatwa katika kipindi cha miaka 11.
.
"Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa kilogramu 157,738.55 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria" alisema Waziri Mhagama.
.
Waziri Mhagama amesema tafiti zinaonesha kwamba, matumizi ya dawa yanaanza katika umri mdogo kati ya miaka 10 na 12. hivyo, Serikali imeona iweke mkazo huko kwani watoto wengi wanapitia katika shule hizo. Pia, elimu imeendelea kutolewa kwenye makundi mbalimbali ya kijamii yakiwemo ya viongozi wa dini, viongozi wa kimila, waandishi wa habari, vyombo vya ulinzi na usalama nk.
.
Kwa upande mwingine, Mhagama amesema Serikali imeendelea kuimarisha huduma kwa kuongeza vituo vya kutolea tiba kwa waraibu kwa kutumia dawa na huduma za unasihi (MAT) ambapo kwa mwaka 2023 kituo kimoja kimefunguliwa mkoani Morogoro katika gereza la kihonda ambapo hadi kufikia mwezi Disemba 2023, jumla ya vituo 16 vilikuwa vinatoa huduma kwa walengwa.
.
Aidha, Waziri Mhagama amesema kumekuwepo na ongezeko la waraibu wanaojiunga na tiba katika kliniki mbalimbali zilizopo nchini, sababu la ongezeko hilo ni kuadimika kwa dawa za kulevya mtaani baada ya kuvunja baadhi ya mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya .
"Takwimu kutoka kwenye vituo vya MAT zinaonesha jumla ya waraibu wapya 2,219 wamejiunga na tiba kwa mwaka 2023 na kufanya idadi ya waraibu wanaopata tiba ya Methadone kufikia 15,915" alisema Mhagama.
#JordanMediaupdates
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

