logo

SERIKALI YAENDELEA KUPIGA HATUA KUPUNGUZA MALARIA NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau imepiga hatua kubwa katika kupunguza ugonjwa wa Malaria kwa kutekeleza afua mbalimbali za kupambana na ugonjwa huo, hali iliyowezesha kuokoa vifo vya akina mama na watoto waliokuwa wanapoteza maisha kutokana na malaria.

‎Mhe. Balozi Kombo ameyasema hayo Juni 28, 2025 jijini Dodoma wakati akitia saini ya mkataba wa uwenyeji kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taasisi ya Umoja wa Wakuu wa Nchi za Afrika (ALMA) dhidi ya Malaria, jijini Dodoma.

‎Amesema Serikali ya Tanzania inaendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika mazalia ya mbu waambukizao Malaria, kinga na tiba lengo likiwa ni kutokomeza kabisa ugonjwa huo.

‎“Vita vya malaria vimegawanyika katika makundi matatu, kwanza kupulizia dawa kwenye mazalia ya mbu, lakini pia kumkinga mwananchi kwa chandarua chenye dawa na tatu ni tiba ya kumpatia mwanachi pindi anapougua malaria, Serikali kupitia wizara ya afya imefanya kazi kubwa sana kwa kupambana kupunguza malaria, sasa hivi ukiuliza mtu mmoja mmoja mara ya mwisho kuugua malaria ni lini utagundua ni zaidi ya miaka hajaugua, hata mimi mwenyewe nina zaidi ya miaka mitano sijaugua malaria, hivyo inatoa takwimu kwa kila mmoja kuwa malaria imepungua kwa kiasi kikubwa sana,” amesema Mhe. Balozi Kombo.

‎Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema, uwepo wa makao makuu ya taasisi ya ALMA nchini kutasaidia kunufaika katika mipango inayopangwa kwa ajilii ya kusaidia nchi za Afrika dhidi ya malaria lakini pia wataalam wa Tanzania kuingia kwenye sekretarieti ya ALMA kujadili mambo mbalimbali yanayohusu malaria.

‎“Pia inaipa nchi yetu hadhi ya kimataifa kwa kuingia mkataba wa uwenyeji na taasisi hii kwa kuiamini nchi yetu na katika mapambano ya malaria Wizara ya Afya kwa kushirikiana na ALMA tutaendelea kuyapa kipaumbele na hatimae kutokomeza malaria ifikapo 2030,” alisema Dkt. Shekalaghe.

‎Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Taasisi ya ALMA, Bi. Joy Phumaphi amesema makubaliano ya nchi mwenyeji yaliyosainiwa leo siyo tu taratibu za kisheria bali ni ishara ya ukuaji endelevu wa ALMA na uongozi wa Tanzania katika diplomasia ya afya ya kikanda na ya bara nzima.

‎“Hapa Tanzania tunajivunia kuchangia katika juhudi za kitaifa za kudhibiti malaria, kuongoza katika uhamasishaji wa rasilimali za ndani kupitia maabara ya kutokomeza malaria Tanzania bara na Zanzibar, na kuboresha matumizi ya takwimu,” alisema.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn