AFCON,CHAN NDANI YA MAFANIKIO YA MIAKA 4 YA DKT.SAMIA
Na Deborah Lemmubi-Dodoma.
Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe Prof. Paramagamba Kabudi amesema kupitia maono na maelekezo ya Dkt.Samia yamefanya kwa mara kwanza tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957 kwa Mashindano ya Mpira wa Miguu kwa Mataifa ya Afrika (AFCON) kufanyika Tanzania mwaka 2027 kwa ushirikiano na Nchi za Kenya na Uganda.
Prof.Kabudi ameyasema hayo wakati akizungumza na Wanahabari leo hii Jijini Dodoma Aprili 14,2025 akielezea mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
Na, kuongeza kuwa mbali ya hayo Tanzania pia imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa Mashindano ya CHAN ambayo yatafanyika mwezi Agosti 2025 ambapo Mashindano haya yatachagiza fursa lukuki ikiwemo ajira kwa vijana.
"Kipekee nimshukuru Mwanamichezo namba moja Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika Sekta ya Michezo. Ambapo kupitia maono na maelekezo yake kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957, Mashindano ya Mpira wa Miguu kwa Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mwaka 2027 yatafanyika Tanzania kwa ushirikiano na nchi za Kenya na Uganda".
"Samabamba na hilo pia tumepata fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya CHAN yatakayofanyika mwezi Agosti, 2025. Mashindano haya yatachagiza kuwapo kwa fursa lukuki za ajira kwa vijana kutokana na ujenzi wa miundombinu, kujenga uchumi pamoja na kuitangaza Tanzania kimataifa kutokana na utalii". alisema.
Aidha, Waziri huyo amesema kuwa Serikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 161.997 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo ikiwa ni maandalizi ya Mashindano hayo, ambapo moja ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Arusha utakaokuwa na uwezo wa kubeba washabiki 32,000.
"Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 161.977 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo ikiwa ni maandalizi ya Mashindano ya AFCON, 2027.
.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Arusha utakaokuwa na uwezo wa kubeba washabiki 32,000; Ukarabati wa uwanja wa Uhuru na Benjamin Mkapa; Ujenzi wa vituo vya mazoezi na kupumzikia wananchi Dar es Salaama na Dodoma; Ujenzi wa Hosteli katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya; Ujenzi wa Akademia ya Michezo Malya; na Ukarabati wa viwanja 5 vya mazoezi.
Aidha, Serikali imeshasaini Mkataba na Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mpya wa Dodoma".
Pia amesema katika kipindi kifupi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali imefanikiwa kutambua na kuenzi Kiswahili kama lugha muhimu kimataifa na hii ni baada ya tarehe7 Julai kutambuliwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kama Siku ya Kiswahili Duniani.
Ambapo uamuzi huu ulifanyika mnamo tarehe 1 Julai, 2024, katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani hii ikidhihirisha uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza na kutangaza Kiswahili katika jukwaa la kimataifa.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

