logo

DORIS MOLLEL FOUNDATION YATOA VIFAA TIBA KWA AJILI YA KUANZISHA WODI YA WATOTO WACHANGA MAHUTUTI - HOSPITALI YA MASIWANI TANGA

Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kushirikiana na Msanii maarufu kutoka hapa nchini Barnaba,leo Disemba 22,2023 imetoa Vifaa Tiba kwa ajili ya kuanzisha Wodi ya Watoto wachanga mahututi (Neonatal Intensive Care Unit) ikiwemo watoto njiti katika Hospitali ya Masiwani, Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Akipokea Vifaa hivyo, Mbunge wa Tanga Mjini na Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu amesema kuwa, mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita kwa Upande wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto ni kujikita katika utoaji wa huduma bora kwa watoto wachanga hususani watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) ili kupunguza vifo vya watoto wachanga.

Mheshimiwa Ummy ameipongeza na kuishukuru Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kuwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu za kuhakikisha Tanzania inafikia Malengo Endelevu ya Milenia ya kupunguza vifo vya watoto wachanga hadi kufikia vifo 12 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2030 kutoka vifo 24 kwa kila vizazi hai 1,000 kwa sasa.

Vifaa tiba hivyo vimetolewa kwa lengo la kupunguza rufaa na kuwasaidia watoto hao kupata huduma bora karibu na jamii alipozaliwa kama alivyoeleza Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Bi.Doris Mollel.

Kulingana na tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa watoto wachanga karibu asilimia 50 hupoteza maisha wanaposafirishwa umbali mrefu kwa sababu ya kupoteza joto la mwili.

Vifaa vilivyotolewa na Doris Mollel Foundation ni pamoja na Vitanda vya hospitali (2),Mashine ya mwanga ya kutibu manjano (1), Mashine ya kusaidia mtoto mchanga kupumua (1), Puto la kumsaidia mtoto kupumua (1),

Mashine ya joto (1), Magodoro ya kuongeza joto la mtoto (10), Mashine za kutolea dawa kusaidia kupumua (3), Mashine ya kupima kiwango cha oxygen kwa mtoto (1), Pump za miguu (5), Pump za umeme (3),Mashine za kutengeneza oxygen (2) na mizani ya kupima uzito wa watoto (2).

Vifaa hivyo vina thamani ya shilingi milioni thelathini na tano (35,000,000/-)

Baada ya kupokea vifaa hivyi, Mhe. Ummy nae amevikabidhi kwa Mkurugenzi wa Jiji la Tanga na kumtaka kuhakikisha Hospitali ya Jiji inaanzisha haraka Wodi ya Watoto Mahututi katika Hospitali hiyo.

Wakati huo huo, Taaasisi ya Mollel imekabidhi zawadi ikiwemo mabeseni ya watoto,kwa wanawake 50 waliojifungua katika Hospitali ya Jiji Masiwani,Kituo cha Afya Makorora, Kituo cha Afya Ngamiani na Kituo cha Afya Mikanjuni.

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn