logo

MOBHARE MATINYI: MAJERUHI 14 WAMEBAKIA HANANG MANYARA

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw.Mobhare Matinyi amesema miili 87 imetambuliwa na kuchukuliwa na familia zao kwa ajili ya mazishi lakini miili miwili ya watoto wa kike wa umri wa mwaka mmoja na miaka mitatu inahitaji vipimo vya vinasaba (DNA) ili kujiridhisha na utambuzi wake na bado utafutaji unaendelea.

.

Matinyi ameyasema hayo leo Disemba 15,2023 jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa fupi kwa waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya hali baada ya maafa ya maporomoko ya tope, mawe, magogo na maji kutoka mlima Hanang wilayani Hanang mkoani Manyara, yaliyotokea alfajiri ya tarehe 3 Disemba, 2023.

Amesema idadi ya majeruhi inaendeelea kupungua Hanang ambapo mpaka hivi sasa wamebakia majeruhi 14 kutoka idadi ya jumla ya 139 waliofikishwa hospitalini baada ya maafa kutokea.

.

"Hadi sasa waathirika 36 ndio waliobakia kambini.Mgawanyo wa waliobakia ni kama ifuatavyo: Shule ya Msingi Ganana ina waathirika 4; Shule ya Msingi Gendabi ina 9 na Shule ya Sekondari Katesh 23" alisema.

Matinyi amesema Serikali inaendelea kuwaunganisha waathirika na ndugu zao na tayari waathirika 460 kutoka kaya 133 wameshaunganishwa na ndugu na jamaa zao hadi kufikia leo.

"Kila mtu au kaya inayoondoka kambini inapewa chakula na mahitaji muhimu ya walau siku 30 ili kuwasaidia waendelee na maisha". alisema Matinyi.

Mkurugenzi huyo amesema kwa kutumia wataalamu wa Wizara ya Afya ambao ni wauguzi wawili na madaktari bingwa watatu wa afya ya akili wakiwa na maafisa ustawi wa jamii 91 kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, jumla ya waathirika 2,144 wameshapata huduma ya afya ya akili na kisaikolojia.

.

Matinyi amesema Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia akaunti ya Mfuko wa Taifa wa Misaada ya Maafa(National Relief Fund)imeshakusanya kiasi cha Sh.149,757,500/= na bado inakusanya.

"Michango ya taasisi na mashirika ya umma kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imefikia shilingi 2,100,000,000/. Hivyo, jumla ya kiasi cha shilingi shilingi 4,749,757,500/= zimeshakusanywa hadi kufikia sasa" alisema Mkurugenzi huyo.

.

Aidha, Mkurugenzi Matinyi amesema Serikali inatoa wito kwa wananchi kutoa misaada zaidi kwenye vifaa vya ujenzi ili viwasaidie waathirika kurejesha hali nzuri katika makazi yaliyoathirika kwa

kuzingatia mapendekezo ya kitaalamu ya eneo jipya.

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn