logo

USIMPE KADI YAKO MTU MWINGINE TUTAIFUNGIA - KONGA

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umetoa tahadhari kwa wanachama wake kwa kuwataka kutumia vizuri kadi zao za matibabu na kuacha kutoa kadi zao kutumika na ndugu zao kwa kuwa ni kosa na kadi hizo zikikamatwa zitafungiwa kupata huduma.

.

Tahadhari hiyo imetolewa Julai 11,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juu ya zoezi la uhakiki wa wanachama na huduma linaloendelea katika vituo mbalimbali vya matibabu nchini.

.

“Naomba niwape tahadhari wanachama wetu, tumebaini wapo wanaowapatia ndugu zao vitambulisho ili wakapate huduma za matibabu, hiyo ni matumizi mabaya ya kadi na katika zoezi hili ambalo tunalifanya tukikukamata tunafunga matumizi ya kadi na kutaka kurejeshwa kwa fedha ambazo zimetumika kwa matibabu isivyo halali,” alisema Konga.

Konga Amesema mambo makubwa yaliyobainika katika zoezi la uhakiki vituoni ni pamoja na matumizi mabaya ya kadi kwa wanachama kutoa kadi zao kwa wasio wanachama wa Mfuko na hivyo kupata huduma kinyume cha Sheria na utaratibu wa Mfuko.

.

“Wapo baadhi ya wanachama wanaacha kadi zao vituoni ambapo jumla ya kadi 2,490 zimepatikana vituoni. Wanachama wanakumbushwa kuondoka na kadi zao mara baada ya kupata huduma na si kuziacha kwani ni kinyume cha utaratibu, niwaombe sana watoa huduma kutoa taarifa ya uwepo wa kadi kupitia Ofisi zetu za Mfuko,” alisema Mkurugenzi Huyo.

.

Kwa upande wa utoaji wa huduma, Konga Alisema imebainika kuwa baadhi ya vituo kutozingatia utaratibu wa uhakiki wa wanachama kabla ya huduma hivyo kuruhusu watu wasiostahili kupata huduma kwa gharama za Mfuko kitendo ambacho hakipaswi kufanyika.

Aidha, Konga amesema kwamba hatua zinazochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na kuzuia matumizi ya kadi 3,589 za wanufaika zilizokuwa na taarifa zenye shaka na kuwataka kufika kuhakiki taarifa zao kama ilivyoelekezwa awali na Mfuko.

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn